RC Arusha Mrisho Gambo aendelea na ziara yake ya kujitambulisha kwa viongozi wa dini jijini Arusha leo
Mh.Gambo amekutana na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania(KKKT)Dayosis ya Kaskazini Kati, Mchungaji Solomon Masangwa , Askofu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God(EAGT) mkoa wa Arusha,Leonard Mwizarubi na Askofu Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana , Dayosisi ya Mount Kilimanjaro.
Katika mazungumzo na viongozi hao kwa nyakati tofauti mbali na kujitambulisha aliwahakikisha dhamira ya serikali kulinda na kuheshimu uhuru na haki ya kuabudu ambayo imekuwepo nchini kwa muda mrefu ikiwa ni njia ya kuwa na taifa la watu wenye hofu ya Mungu.
Alisema kutokana na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dr. John Joseph Pombe Magufuli kutaka kuwainua wananchi wa chini kupitia mapato ya ndani halmashauri zimetenga asilimia 10 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa Wanawake na Vijana wajasiriamali zitakazowawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali, hivyo wawajulishe waumini wa dini zote na serikali iko tayari kupanga utaratibu wa maafisa maendeleo ya Jamii na Vijana kupita na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na madhehebu ya dini hii iwe inufaishe watu wote katika Mkoa huu bila kujali itikadi za kidini wala kisiasa.
Askofu Stanley Hotay aliupongeza uongozi wa mkoa kuimarisha hali ya utulivu na kuomba vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo Mkuu wa mkoa ndiye Mwenyekiti wake kukabiliana na changamoto za kiusalama na viashiria vya uvunjifu wa amani. Pia amependezwa nja utaratibu huu kwa Mkuu wa Mkoa kuwatembelea viongozi mbalimbali wa dini ili kushauriana masuala mbalimbali yanayohusu Mkoa wetu.
Aidha alishauri kutokana na idadi ya watu wanaotumia usafiri wa anga kuongezeka kuna haja ya Serikali kufikiria uwezekano wa kupanua zaidi uwanja wa ndege wa Arusha uliopo Kisongo ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa badala ya kutegemea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) pekee.
Mh. Gambo amewahakikishia viongozi hao kuwa serikali itakua ikiwashirikisha mipango mbalimbali inayokusudia kuitekeleza ili watoe mawazo yao katika kuiboresha na kuifanya itekelezeke kwa wepesi zaidi.
Comments
Post a Comment