Mbowe: Sidaiwi na NHC, Namiliki Jengo kwa Asilimia 75 Kuanzia Mwaka 1997


 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Freeman Mbowe amekana kudaiwa kiasi chochote na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akisema katika jengo hilo la Bilicanas la jijini Dar es Salaam, yeye si mpangaji bali ni mmiliki mwenza wa NHC.

Alisema anamiliki jengo hilo kwa asilimia 75 tangu mwaka 1997 na kinachofanywa na shirika hilo la umma kinasimamiwa na viongozi wa dola kwa kuwa yeye ni mpinzani.

“Mimi sidaiwi na NHC na madai yanayofanyika hayapo kisheria bali ni uharibifu wa makusudi unaolenga kunikomoa ambao unatokana na msimamo wangu kisiasa” alisema Mbowe.

Alisema kuzongwazongwa huko ni kwa kuwa yeye ni mpinzani na kabla upinzani haujawa mkubwa alikuwa hafanyiwi hivyo.

Kama ni kudaiwa, Serikali ina madeni, wafanyabiashara wana madeni lakini hawajafanyiwa kama anachofanyiwa Mbowe. Kwa nini Freemedia iwe ya kwanza kushambuliwa kwa kutoa kompyuta zake nje na kujaribu zake nje na kujaribu kuzikagua kwa ndani zina nini? Mbowe alihoji.

Aliongeza kuwa si lazima kutoa vitu vya mdaiwa nje, bali vinaweza vikafungiwa ndani akapewa muda wa kulipa deni analodaiwa na anaposhindwa ndipo vitu vinapigwa mnada vikiwa mlemle ndani.

“Kama si siasa za majitaka inawezekana vipi deni mpaka kufikia zaidi ya bilioni na kwa kodi ipi ambayo nilitakiwa kulipa kwa mwaka au kwa mwezi?” alihoji huku akisema alianza kumiliki jengo hilo tangu mwaka 1997 hata kabla hajawa Mbunge wala mwenyekiti wa CHADEMA.

“Wanachokifanya ni kutokuheshimu mikataba na nyaraka za kisheria zinazoonyesha umiliki wangu katika jengo hilo, lakini vielelezo vyote ninavyo na haki yangu nitaipata mahakamani” alisema Mbowe

Kadhalika alisema nina miradi mingi ndani na nje ya nchi na kudhibiti mradi mmoja haikwamishi nia yake ya kupigania haki. “Hata maandiko yanasema mtu hataishi kwa mkate pekee” alisema.

Alipoulizwa kwamba kulikuwa na kesi ambayo ameshindwa kama inavyoelezwa na Serikali na Uongozi wa NHC, Mbowe alisema “waulize hiyo kesi namba ngapi na ya lini. Jambo zito kama hilo linawezekanaje kuwa na kesi na wahusika wasifahamu? Tusubiri tuone”.

Hivi karibuni Ofisi za Gazeti la Tanzania Daima linalomilikiwa na Mbowe, zilizokuwa kwenye jengo la NHC maarufu kama Bilicanas vyombo vyake vilitolewa nje na madalali wa shirika hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa Mbowe anadaiwa sh. bilioni 1.6 kama pango ya jengo hilo.

Comments

Popular posts from this blog

UFUGAJI BORA WA KUKU WA KIENYEJI

YANGA YAPATA PIGO, KIPA WAKE NAMBA MOJA DEO MUNISHI AFIWA NA BABA YAKE

Kwa Nini Watu Wengi Wanaamini Uchawi Unaleta Mafanikio?