Azam nayo yaanza kulia na waamuzi Ligi Kuu Bara
Kocha Zeben amesema, changamoto kwa upande wa waamuzi imekuwa ikijirudia kila kukicha na siyo kwa sababu ya mchezo unaochezwa uwanjani, bali maamuzi yanaathiri klabu kama klabu, wachezaji wenyewe na hata makocha ambao wanakuwa wamejiandaa kwa ajili ya kupambana lakini mwisho wa siku waamuzi wanaharibu mchezo husika.
Kauli ya Hernandez imekuja saa chache mara baada ya Azam FC kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar hapo usiku wa jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Chamazi Complex jijini Dar es salaam.
Mtibwa Sugar ndiyo ilianza kuwa mbele kwenye mchezo huo baada ya kufunga bao la kushtukiza katika dakika ya pili likifungwa na Rashid Mandawa kabla ya nahodha wa Azam FC kwenye mchezo huo, Himid Mao, kusawazisha kwa mkwaju wa penalti kufuatia Henry Joseph, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
“Tunasikitishwa sana na maamuzi ya waamuzi, kwa muda mrefu kutokea tumekuja hapa hatujawahi kuzungumzia tatizo hilo, hili ni tatizo kubwa limekuwa likijirudia kila kukicha, inaonekana kwamba kuna kampeni fulani waamuzi wanapewa nafasi wafanye labda kwa sababu ya Azam FC, lakini lazima watambue kuwa hii sio haki."amesema, Hernandez.
Mchezo huo ulichezeshwa na waamuzi Israel Nkongo na wasaidizi wake Frank Komba na Soud Lila.
Comments
Post a Comment